Mariam Masenga ''Wengine Wanasema Corona Haiwapati Watu Weusi Hivyo Wanakataa Kunawa Mpaka Walazimishwe na Uongozi tu ''


Na. Mwandishi wetu, DODOMA

PAMOJA na kutolewa kwa elimu mbalimbali na viongozi wa serikali juu ya kujikinga na virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari duniani wa CORONA bado jamii imekuwa na fikra hasi kwa madai kuwa watu weusi hawawezi kukumbwa na ugonjwa huo.

Hali hiyo imebainishwa na   Mariam Masenga ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa kuwataka wateja na wafanyabiashara kunawa mikono kwa maji na sabuni katika soko la Bonanza lililopo Jijini Dodoma  maarufu kwa kuuza Samaki, Mbogamboga na Matunda .

Akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa anakumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukutana na baadhi ya watu ambao wanakuwa wabishi kunawa mikono kwa madai kuwa watu weusi kamwe ugonjwa huo wa Corona hawawezi kupatwa. 

“Kunatakiwa elimu kubwa sana kwa jamii mimi nipo  hapa  mlangoni ambako uingia wateja na wafanyabiashara wengi kwa ajili ya kusimamia watu kunawa mikono changamoto iliyopo ni kwamba wapo wengine ambao ni wabishi wanakataa kunawa wakidai kuwa eti wananawa kwani kuna chakula? wengine wanasema eti Corona haiwapati watu weusi hivyo wanakataa kunawa mpaka walazimishwe na uongozi tu.

“Na sijui nani katoa elimu kuwa watu weusi hawawezi kupatwa na ugonjwa huu wa Corona, serikali na wataalamu wa afya wanatakiwa kutoa elimu ya kutosha ili kuondosha ukakasi huo ambao unaopotosha ambao unaendelea kuvumishwa kuwa watu weusi hawawezi kupatwa na Corona” alisema Mariam.

Hata hivyo kutokana na na kuwepo kwa tishio la ugonjwa hatari unaotokana na maambukizi ya virusi vya CORONA wafanyabiashara na wateja wa Soko la Bonanza katika jiji la Dodoma wametakiwa kuzingatia utumiaji wa vitakatisha mikono pindi wanapoingia sokoni  kufanya biashara au kununua bidhaa na yeyote atakayeonekana kukaidi hataruhusiwa kuingia ndani ya soko hilo.

Hayo yamelezwa na Katibu  mkuu wa soko hilo, Dickson Mwesigwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea soko hilo kwa ajili ya kuangalia taratibu za utumiaji wa vitakatisha mikono kwa ajili ya kujikinga na gonjwa hatari linalosababishwa na virusi vya Corona unafuatwa.

Mwesigwa alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa ugonjwa huo ambao ni tishio kwa dunia uongozi wa soko umelazimika kuweka vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vitakatisha mikono katika milango miwili ya soko na kuwaweka wasimamizi ambao wahatahakikisha kila anayeingia sokoni hapo ananawa mikono kwa kuzingatia maelekezo ya serikali na wataalamu wa afya kwa ujumla.

Alisema kuwa vifaa hivyo ambavyo vimwekwa katika milango maalumu ya kuingilia katika soko hilo na kuwaweka wasimamizi ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha ananawa mikono pindi anapotaka kuingia ndani ya soko na bila kujali anayeingia sokoni ni mfanya biashara au ni mteja.

“Sokoni tunapokea watu wengi, huwezi kujua nani mwathirika na ni nani ambaye yupo salama kutokana na hali hiyo uongozi wa soko la bonanza ambalo ni maarufu kwa kuuza samaki, matunda na mbogamboga ,tumeamua kutekeleza kwa vitendo maagizo ya serikali na wataalamu wa afya kwa kuweka vifaa mbalimbali vya kujikinga na ugonjwa huo.

“Katika soko kuna milango miwili ya kuingilia na kila mlango tumeweka vitakatisha mikono na tumeweka watu wa kusimamia haijalishi wewew ni mfanyabiashara au ni mteja nilazima kunawa mikono kwa sababuni na maji tililika kwa afya ya mtu mwenyewe na kwa usalama wa watu wote waliopo sokoni” alisema Katibu Mwesigwa.

Hakizungumzia hali ya biashara Mwesigwa alisema kuwa baada ya kutokea ugonjwa huo biashara ilionekana kuzorota kutokana na jamii jujawa hofu na kudhani kuwa maambukizi ya Corona yanatokana na hewa.

“Kabla ya serikali kufunga shule, vyuo vya elimu ya juu na kati pamoja na kutangaza aina ya mikusanyiko isiyotakiwa hali ilikuwa mbaya sana sokoni watu walikuwa hawaji kununua bidhaa, lakini baada ya serikali kutangaza kufunga vyuo , shule za msingi na kutangaza aina ya mikusanyiko na kuyaacha masoko bila kuyafunga angalau sasa wateja wameweza kuja sokoni angalau biashara imeanza kuwa nzuri japo siyo sana na mzunguko wa   hela kwa sasa ni mdogo” alieleza Mwesigwa.

MWISHO    

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.