Na Mwandishi Wetu ,Dodoma
MTU mmoja anayesadikiwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35 amezama
kwenye maji wakati akivua samaki katika eneo la bonde la Mpunga Bahi Makulu
Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma mpaka sasa juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Akithibitisha taarifa hizo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi
Mukunda amewataka wananchi kuchukua tahadhari na kuacha kufanya shughuli zao
kwenye maeneo hatarishi.
“Ni kweli tukio hilo limetokea ni jambo la kusikitisha sana,
tumeshawaelekeza wananchi mabonde mengi yamejaa maji ni hatari kwa maisha
yao,” alisema
Pia aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhali kuifuatia
mvua zinazoendelea kunyesha.
Alisema mito mingi imekuwa ikiishia katika wilaya ya Bahi hali
ambayo inasababisha maji kuingia kwenye makazi ya watu na kwenye mashamba.
Aidha alitoa tahadhali kwa wazazi kuhakikisha watoto wao wako
mahali salama kutokana na baadhi ya watoto kuonekana kwenye mito na madimbwi
yaliyojaa maji wakiogolea.
Diwani wa kata ya Bahi Augustine Ndonu alisema tukio l mtu
kuzama limetokea juzi, saa kumi jioni maeneo ya mashamba mapya ambapo mtu
huyu mwanaume alizama wakati akivua samaki aina ya kambale na mpaka sasa bado
hajapatikana na juhudi za kumtafuta inaendelea.
Alisema taarifa ilishatolewa kituo cha polii na juhudi a
kumtafuta bado zinaendelea.
Alisema tahadhali inaendelea kutolewa katika ofisi za
kijiji, kuwataka watu anaokwenda kuvua samaki waende kwa makundi na si kila
mmoja kwenda peke yake kwani maji ni mengi.
Alisema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na mvua
iliyonyesha jana na juzi maji yamejaa na kufunika mashamba ya mpunga na hivyo
kupelekea maeneo ya mabonde ya mpunga kuwa na maji na matope mengi jambo ambalo
ni hatari kwa usalama wa wananchi wanaojihusisha na uvuvi wa samaki.
Alisema mito mingi iliyopo Bahi, mto Bubu ambaozhutokea Kondoa,
Mto Chikola na Sanza Manyoni yote hupeleka maji kwenye bwawa la tope la
Bahi.
“Hapa Bahi maji yamejaa sana na watu wengine walishindwa kupanda
mpunga kutokana na maji kujaa sana na watu wamekuwa wakitumia fura hiyo kufanya
uvuvi wa samaki jambo hilo ni hatari kwani maji na tope ni jingi,” alisema.
Aliwataka wananchi kucukua tahadhari hasa katika kipindi hiki
cha mvua
Mwisho
Comments
Post a Comment