Na. Mwandishi Wetu,
Waziri wa Afya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu leo ametoa
taarifa ya mwenendo juu ya mlipuko wa ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu
inayosababishwa na virusi vipya jamii ya Corona (COVID-19) ikiwa ni muendelezo
wa taarifa tunazotoa mara kwa mara wakati wa milipuko.
Waziri Ummy Mwalimu (katikati) |
Katika taarifa hiyo,
Waziri Mwalimu amesema idadi ya wagonjwa duniani imeendelea kuongezeka ambapo
hadi kufikia tarehe 27 Februari, 2020 jumla ya watu 83, 652 wamethibitika
kuugua, na kati ya hao wagonjwa 2,858 wamefariki. Asilimia 94 ya wagonjwa waliothibitika
duniani wapo nchini China. Hadi sasa jumla ya nchi 51 zimeripoti ugonjwa huu
ambapo kati ya hizo tatu ni nchi za Afrika ambazo ni Algeria, Nigeria na
Misri.
Awemewatoa wasiwasi
wananchi kuwa hadi sasa Tanzania haina mshukiwa wala mgonjwa wa ugonjwa wa
kirusi cha corona (COVID-19). Hata hivyo, bado nasisitiza kuwa tunahitaji
kuendelea kuchukua Tahadhari kubwa ya kujikinga kupata ugonjwa huu kutokana na
kuwa na muingiliano wa wasafiri kati ya Tanzania na mataifa mengine
yaliyoathirika.
Ameongeza katika
taarifa hiyo kuwa kutokana na hatari iliyopo ya maambukizi ya ugonjwa huu,
Serikali imejiandaa kukabiliana na tishio la ugonjwa huu, hususan kupitia
maandalizi ya muda mrefu ambayo tumekuwa tukiyafanya kukabiliana na
magonjwa hatari ya kuambukiza. Hatua mbalimbali tayari zimechukuliwa, na
zinaendelea kuchukuliwa ambazo ni pamoja na:
Kuendelea na
uchunguzi na ufuatiliaji wa wasafiri wote wanaoingia nchini kwenye mipaka yetu
ikiwemo viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu. Kwa kipindi cha
kuanzia Januari 30 hadi 27 Februari mwaka huu, jumla ya wasafiri 11,048
wamechunguzwa katika mipaka yetu ambao wanatokea katika nchi zilizo na ugonjwa
huu kwa sasa ikiwamo China. Wizara inavyo vipima joto 140 (vya mkono 125
(hand-held thermo scanners) na vya kupima watu wengi kwa mpigo 15 (Walkthrough
thermoscanners)) ambavyo vimefungwa na vinatumika katika maeneo yetu ya
mipakani ikiwemo viwanja vya ndege na bandari.
Vilevile,
tumeongeza idadi ya wataalamu wa afya katika maeneo ya mipakani ikiwa ni pamoja
na kuajiri watumishi 100 ili kuimarisha ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia
nchini kupitia maeneo ya mipakani.
Tumeandaa dawa,
vifaa kinga na vitakasa mikono (Alcohol-based sanitizers) ambavyo tayari vipo
kwenye Bohari za Dawa za Kanda kwa ajili ya kutumika endapo kutatokea mgonjwa.
Tumeandaa maeneo
maalum katika mikoa yenye uwezekano mkubwa wa kupata wagonjwa kwa ajili ya
kuwaweka washukiwa na kuwapatia matibabu wagonjwa.
Serikali
imeimarisha uwezo wa kupima sampuli kupitia Maabara yetu ya Taifa ya Afya ya
Jamii kwa watu wote wanaohisiwa kuwa na viashiria au dalili za ugonjwa huu
ambapo ndani ya masaa 4 – 6 tunaweza kutoa majibu ya vipimo.
Tumeendelea kutoa
elimu ya afya kwa umma kupitia njia mbalimbali ili wananchi na watoa huduma
waendelee kuchukua tahadhari.
Pia, tumetoa
mafunzo kwa watumishi wa sekta ya afya katika kukabiliana na magonjwa ya
milipuko na majanga ikiwemo jinsi ya kutoa matibabu ya magonjwa ya milipuko,
kuchukua sampuli, uelimishaji na kuzingatia kanuni za afya.
Wizara imeisha
waelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kubainisha vituo vya kutolea
matibabu kwa washukiwa/wagonjwa wa covid-19 endapo watatokea ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha kwamba vituo hivi vina vifaa vyote muhimu vya kutolea huduma.
Ugonjwa huu
huenezwa kwa njia ya majimaji yatokayo njia ya hewa wakati mtu mwenye ugonjwa
huu anapokohoa au kupiga chafya, kugusa majimaji yanayotoka puani (kamasi),
kugusa vitambaa au nguo zilizotumiwa na mtu aliyepata maambukizi ya ugonjwa huu
au maeneo mengine yaliyoguswa na mtu mwenye virusi vya ugonjwa huu.
Hivyo ni muhimu kwa
kila mwananchi kufanya yafuatayo ili kuzuia ugonjwa huu usiingie nchini:-
Kufuata kanuni za
Afya kwa kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kitambaa safi au nguo
uliyovaa sehemu za mikono (Kiwiko cha mkono kuzuia hewa/makohozi kusambaa na
kuhatarisha wengine).
Kuzingatia usafi
binafsi ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa
mikono.
Kujizua kupeana
mikono na kukumbatiana.
Kuepuka kugusana na
mgonjwa mwenye dalili za magonjwa ya njia ya hewa mwenye historia ya kusafiri
maeneo au nchi zilizoathirika na ugonjwa huu.
Kuwahi kwenye kituo
cha kutolea huduma za afya endapo utakuwa na dalili za ugonjwa huu.
Kutoa taarifa ya
uwepo wa mtu mwenye dalili zinazohiswa kuwa za ugonjwa huu kwenye kituo cha
huduma za afya kilicho karibu nawe au piga simu namba 0800110124 au 0800110125
bila malipo.
Kusubiri au kuepuka
safari zisizo za lazima kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika na inapolazimu
kusafiri, wasafiri wanapaswa wapate maelezo ya kitaalamu kabla ya kuondoka
nchini. Kwa wale ambao wanafanya biashara, tunashauri wafanye biashara
mtandao katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa huu.
Aidha, Serikali
inatoa maelekezo kwa Mikoa yote nchini kufanya yafuatayo:
Kuhakikisha ndani
ya siku tatu wanawasilisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya jina la kituo
ambacho kimetengwa maalum kwa ajili ya kuhudumia washukiwa au wagonjwa endapo
watatokea katika kila Halmashauri.
Waziri Ummy Mwalimu (kulia) |
Kuhakikisha
Hospitali zote, za umma na binafsi, zilizoko katika maeneo yao zina eneo la
muda la kumshikilia mshukiwa.
Kuimarisha
uzingatiwaji wa Kanuni za kuzuia maambukizi (Infection Prevention and Control-
IPC) kwa kuhakikisha watumishi wanahimizwa na wanapatiwa vifaa vinavyohitajika.
Aidha, Mikoa
ihakikishe uwepo wa vitakasa mikono katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu
ikiwemo mahoteli, nyumba za wageni, sehemu za ibada, shule, ofisi, sehemu za
kazi na biashara.
Ameongeza kuwa
Serikali imeendelea kufanya mawasiliano kwa karibu na serikali ya China kuhusiana
na watanzania 504 ikiwepo Wanafunzi waliopo mji wa Wuhan. Ninapenda kuwaondoa
wasiwasi kuwa watanzania hawa wapo kwenye mikono salama. Hatua mbalimbali
zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha wako salama na mahitaji yao muhimu
wanapatiwa.
Akihitimisha taarifa
hiyo ameendelea kusisitiza kuwa ushirikiano wa pamoja wa wananchi, sekta na
wadau mbalimbali katika kuzuia na kukabiliana na mlipuko huu ni muhimu. Hii ni
pamoja na wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kipindi hiki ambacho bado ugonjwa
huu haujadhibitiwa na unaendelea kusambaa katika mataifa mengi.
Amesema serikali
inaendelea kufuatilia kwa umakini mkubwa hali ilivyo duniani na endapo
itatengamaa tutawajulisha haraka. Nitoe rai kwa wananchi kutosambaza taarifa
ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika.
Akimalizia kutoa
taarifa hiyo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali
wa sekta ya afya, likiwemo shirika la Afya Duniani (WHO) na sekta ya habari
katika kuhakikisha kuwa afya za wananchi zinalindwa na elimu ya kutosha inatolewa.
Comments
Post a Comment