POLISI DODOMA WAELEKEZA ASKARI WOTE KAMPUNI BINAFSI KUPITIA MAFUNZO


Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Jeshi la Polisi nchini limesema askari wote wa kampuni binafsi ambao watakuwa hawajapatiwa mafunzo ya kazi zao hawataruhusiwa kujihusisha na kazi za ulinzi ifikapo Desemba mwaka huu.
 
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Narsis Msama
Hayo yamebainishwa hii leo Februari 28, 2020 na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Narsis Msama katika kikao cha wamiliki na wakurugenzi wa makampuni binafsi ya ulinzi nchini.

Amesema endapo wahusika hawatafanikisha suala la kuwapatia mafunzo wafanyakazi wao ni wazi kuwa watawazuia kuingia katika lindo kwani itakuwa ni kinyume na maazimio ya kikao hicho kwa mujibu wa sheria za nchi.

"Kampuni ya ulinzi isiyotoa mafunzo kwa wafanyakazi wake ina maana sisi tutamzuia mlinzi wake kufanya kazi na hii ina maana kampuni itakuwa imezuiwa pia kufanya kazi mpaka pale watakapokamilisha taratibu husika," amefafanua Kamishna Msama.

Awali akiongea katika kikao hicho Mkurugenzi wa miradi wa Kampuni ya Data Vision International, Macmilan George amesema kwa ushirikiano wa wadau wa sekta binafsi ya Ulinzi na Jeshi la Polisi wamebuni mfumo wa kusimamia sekta ya ulinzi nchini.

Amesema mbali na hatua hiyo ambayo inakumbusha juu ya umuhimu wa utunzaji wa taarifa za makampuni pia mkutano huo umezindua rasmi utaratibu huo kwa kukutana na wakuruhenzi hao makampuni binafsi 60 yanayotoa huduma za ulinzi Jijini Dodoma. 

"Mfumo huu ni wazi kuwa utaratibu utunzaji wa kumbukumbu na taarifa mbalimbali katika sekta binafsi ya ulinzi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na ndio maana leo tumekutana hapa Dodoma na wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi," amesema Goerge.
 
Mkurugenzi wa miradi wa Kampuni ya Data Vision International, Macmilan George
Aidha, amebainisha kuwa mfumo huo pia utasaidia  kuhifadhi taarifa za watumishi wa sekta ya ulinzi binafsi ili kupunguza vitendo vya uachaji kazi holela na matukio ya uhalifu hakikiwemo masuala ya taarifa za afya na kifedha.

George ameongeza kuwa lengo kubwa la ubunifu wa mradi huo ni kuisaidia serikali katika kuratibu sekta ya ulinzi binafsi katika masuala ya kijamii kwa kuweka mikakati endelevu itakayosaidia kufikia malengo.

"Kama mnavyojua nchi haiwezi kuendelea au kupata maendeleo iwapo hakuna sekta ya ulinzi ambayo ni imara na ili uwe imara unahitaji mipango thabiti ya kimkakati ili kujiimarisha na kuleta matokeo chanya," amefafanua Mkurugenzi George.

Naye Mkaguzi mstaafu wa Jeshi la Polisi George Nelson Andala ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni binafsi ya ulinzi akizungumzia hatua hiyo amesema wameipokea kwa mtazamo chanya na wana imani itawasaidia katika mambo muhimu hasa taarifa za askari wao.

Amesema mradi huo ambao pia ni wa kuwasajili askari na watumishi katika sekta binafsi sio tu utawasajili na kutunza kumbukumbu bali pia utasaifia kuondoa dhana ya watumishi kuacha kazi kiholela na kuhama kampuni. 

"Utunzaji huu wa kumbukumbu na usajili utawafanya askari kutambulika na hata kukopesheka na taasisi mbalimbali za kifedha kwakua taarifa zao zitakua ni halali na zenye uthibitisho wa mamlaka mbalimbali za kiserikali," amefafanua Andala.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.