JAMII YATAKIWA KUCHANGIA UENDELEZAJI WA SAYANSI NA TEKNOLOJIA NCHINI


Na. Dennis Gondwe, DODOMA
JAMII imeshauriwa kujitokeza na kuchangia juu ya uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kukuza ubunifu na kuongeza ajira nchini.
Prof. Maulilio Kipanyula akionesha Mwongozo wa MAKASATU -2020 kwa waandishi wa habari
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Maulilio Kipanyula katika kikao kazi na waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma juu ya mashindano ya kitaifa ya sayansi, teknolojia na ubunifu (MAKISATU) katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma leo.

Prof. Kipanyula amesema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina jukumu la kuratibu na kusimamia utafiti na ubunifu katika fani za Sayansi na Teknolojia. Katika kutekeleza jukumu hilo, Wizara imeandaa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) ili kuchochea ukuaji na maendeleo katika fani ya Sayansi na Teknolojia nchini. Katika eneo hilo, alitoa wito kwa jamii kuona umuhimu wa kuendeleza Sayansi na Ubunifu kwa kujitokeza na kuchangia michango mablimbali. 

“Wadau wakijitokeza kuchangia juu ya uendelezaji wa Sayansi na Ubunifu watachangia kukuza ubunifu na kuongeza ajira nchini. Mtu mmoja mmoja, mashirika au taasisi zijitokeze kutuunga mkono” alisema Prof. Kipanyula.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sylvia Lupembe alisema kuwa waandishi wa habari ni kundi muhimu katika kufanikisha mashindano ya MAKISATU mwaka 2020. “Kutokana na umuhimu wa wana habari katika kufikia malengo ya Wizara katika MAKISATU, tumeona tukutane hapa ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu jukumu la Wizara la kusimamia na kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini” alisema Lupembe.
Sylvia Lupembe (kushoto) akifafanua jambo
Aidha, aliwataka wanahabari hao kuandika habari za MAKISATU kwamapana yake ili kuchochea hamasa katika jamii na kukuza Sayansi na ubunifu.

Mshiriki katika kikao kazi hicho, Anneth Andrew ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuandaa kikao kazi na waandishi wa habari. “Kikao hiki kimetuweka pamoja. Hii ni heshika kwetu. Sisi tupo tayari kutoa ushirikiano wetu kufanikisha mashindano haya” alisema Andrew.
Mshiriki Anneth Andrew akiahidi ushirikiano 

Mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini yatafanyika kuanzia tarehe 16-20 Machi, 2020 katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, yakiwa yanafanyika kwa mara ya pili mfululizo.

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.