WAZIRI ZUNGU AWATAKA WATUMISHI OFISI YAKE KUWAJIBIKA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu amemtaka kila mtumishi katika Ofisi hiyo kuwajibika ipasavyo mahali pa kazi na kuepuka kujihusisha na vitendo visivyokuwa vya kimaadili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo
Zungu ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo ambapo aliwakumbusha kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kuimarisha utendaji kazi ili kufanikisha dhana ya Tanzania ya viwanda.

“Ninafahamu kwamba watumishi wana malalamiko yanayohusu kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu na upungufu wa watumishi katika Idara na Vitengo, malalamiko haya ni mtambuka katika Wizara zote kwani yametokana na uhakiki wa vyeti vya elimu ya sekondari na ualimu zoezi lililoendeshwa na Serikali kuanzia mwaka 2016. Ninawasihi muwe na subira wakati Serikali ikiimarisha mifumo yake ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu,” alisisitiza.

Aidha, Waziri Zungu alibainisha kuwa Baraza la wafanyakazi ni jukwaa muhimu mahali pa kazi kwani ni kiunganishi kati ya Menejimenti na Wafanyakazi hivyo aliwataka kuendeleza ushirikiano ili kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Ofisi na Taifakwa ujumla.

“Watumishi wenzangu hakikisheni mshahara mnaopewa mnautendea haki! Msitake kupata mshahara wa bure! Fanyeni kazi kwa bidii” Zungu alisisitiza.

Aliongeza kuwa kuwepo kwa Mabaraza ya Wafanyakazi katika Taasisi ni takwa la Kisheria kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi za Idara na Ofisi ambapo malengo yake ni  kuhakikisha kuwa majukumu yanatekelezwa ipasavyo, kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga mazingira bora ya kazi, maslahi ya watumishi na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi.

Aliwakumbusha kuwa wajibu wa Mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na kuzingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo baada ya kufungua mkutano 
Agenda na madhumuni ya mkutano huu ni kutoa Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kipindi cha nusu mwaka cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2019/20.

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.