Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Naibu Meya aliyemaliza muda wake Jiji
la Dodoma, Jumanne Ngede amesema kuwa wazazi na walezi wa Kata ya Chamwino
jijini Dodoma wenye wanafunzi wanaosoma elimu ya msingi na sekondari ambao ni
watoro hawatavumiliwa, badala yake wataburuzwa kwenye vyombo vya sheria ikiwemo
mahakamani.
Ngede amesema hayo alipokuwa
akizungumza na wajumbe wa kamati ya bodi ya shule ya msingi ya Chinangali
kwenye kikao cha kutadhimini changamoto mbalimbali zinazokabili shule zilizopo
kwenye kata hiyo ikiwemo za sekondari na msingi kuhusiana na utoro wa wanafunzi
na miundombinu yake.
Ngede ambaye pia ni Diwani wa Kata
hiyo amesema hayo kuwa hatua ya kuwaburuza mahakamani wazazi na walezi, ina
malengo ya kuziona shule hizo zilizopo kwenye Kata hiyo zinafanya vizuri kwenye
kitaaluma na watoto wanaosoma wale wa msingi na sekondari wanafanya vizuri
kwenye kielimu pindi wanapohitimu elimu yao.
Alisema serikali kwa hivi sasa
imewapunguzia makali na mzigo mkubwa kwa upande wa elimu hivyo hakuna
sababu kwa wazazi na walezi kuwavumbia macho watoto wao ambao wamekuwa na tabia
ya utoro na wao kushindwa kutoa ushirikiano kwa walimu husika na kamati
zilizochaguliwa kwenye shule zao.
“Ili tuweze kufika katika ushindani
wa kufanya vizuri kitaaluma kwenye Wilaya yetu hii ya Dodoma ni vema wazazi, walezi,
walimu na kamati ya bodi ya shule iliyochaguliwa wakao kitu kimoja ambacho
kitakachowezesha kukomesha tabia na pia kutoa elimu kwa baadhi ya wazazi ambao
watoto wao wamekuwa watoro” alisema.
Kwa upande wake Afisa elimu kata ya
Chamwino Sponsa Mkusa alisema pamoja na serikali kuwapunguzia baadhi ya
mahitaji ya wanayohitaji kwa wanafunzi, bado wana wajibu wa kuhakikisha
wanachangia elimu hiyo ikiwemo katika eneo la chakula na mahitaji mengineyo
ambayo yanayohusiana na mzazi na mlezi.
Mkusa alisema kuna baadhi ya
mahitaji hayahusiani na serikali kama vile ununuzi wa madaftali,chakula na sare
ya shule,hivyo ni lazima wazazi na walezi lazima muhusike katika kuhakikisha
watoto hao wanasoma vizuri badala ya kusubiri serikali iwapatie.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya shule ya
msingi ya Chinangali alisema kuwa pamoja na hatua ya kuwachukulia wazazi na
walezi wenye watoto ambao ni watoro,pia shule hiyo inakabiliwa na ukosefu wa
madawati ikiwemo na vyumba suala ambalo limekuwa likisababisha walio wengi
kukosa sehemu ya kukaa.
MWISHO
Comments
Post a Comment