Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imeongeza umakini katika utoaji wa vitambulisho vya
Taifa katika mikoa iliyopo mipakani na hivyo kuwataka watanzania kusaidia
kuwatambua watu wasio raia wa Tanzania ambao wanachukua vitambulisho vya uraia
ili kudhibiti hali ya ulinzi na usalama ndani ya nchi.
Waziri Mkuu amesema
hayo leo bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo
wakati akijibu swali la mbunge wa Buhigwe, Obama Ntabaliba aliyetaka kujua
kauli ya serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata vitambulisho vya NIDA.
Amesema upo ukweli
kwamba watanzania wengi walikuwa hajawafikiwa kupata vitambulisho vya Nida
mpaka ngazi ya vijiji na vitongojini jambo ambalo serikali imelifanyia kazi kwa
kuongeza idadi ya watumishi kwenye ngazi za halmashauri ili kuweza kufika
kwenye vijiji na vitongoji.
Aidha, amesema
serikali imeridhia kutumika kwa namba ya kitambulisho pale palipo na uhitaji
kama mwananchi atakuwa hajapata kitambulisho na kusisitiza utekelezaji wa
maelekezo waliyotoa ikiwemo kubandikwa orodha ya wananchi na namba zao ili
kuweka urahisi wa upatikanaji wa namba hizo kwa wananchi.
MWISHO
Comments
Post a Comment