Na. Amiri Kilagalila, NJOMBE
Jitihada za makusudi zimetakiwa
kuchukuliwa ili kuondoa sifuri na daraja la nne kwenye mitihani ya kidato cha
nne katika shule za Halmashauri ya Mji wa Njombe licha ya Halmashauri hiyo
kushika nafasi ya pili kwa ufaulu katika Mkoa wa Njombe.
Katika kikao cha Baraza la Madiwani
la Halmashauri ya Mji wa Njombe baadhi ya madiwani akiwemo Abuu Mtamike wa Kata
ya Mjimwema,Filoteus Mligo Diwani wa Kata ya Lugenge na Reginald Danda
toka Kata ya Iwungilo wamesema wao kama madiwani wamekuwa wakihamasisha jamii
kutekeleza yale yanayowapasa katika kukuza elimu hatua ambayo inapaswa kuungwa
mkono na serikali kwa kupeleka fedha za maendeleo na kununua madawati badala ya
kusalia wakipongezana kwa kushika nafasi ya pili kimkoa.
Awali akitoa salaam za serikali Mkuu
wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri amesema Halmashauri ya Mji wa Njombe licha ya
kufanya vizuri bado inapaswa kuongeza nguvu katika sekta ya elimu kwani bado
kuna wanafunzi wanafeli mitihani yao.
Mwenyekiti wa kamati ya afya uchumi
na elimu katika Halmashauri hiyo, Yurick Msemwa ambaye ni Diwani wa Kata ya
Luponde amesema ili kupandisha kiwango cha ufaulu zaidi, mshikamano wa pamoja
unahitajika kwa kila mmoja ndani ya Halmashauri hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Mji wa Njombe, Iluminata Mwenda amesema wamelazimika kuanzisha kampeni ya
kuondoa zero katika shule zote kwa kuboresha miundombinu ya elimu na mbinu za
ufundishaji.
Katika matokeo ya kidato cha nne
kwa mwaka 2019 Halmashauri ya Mji wa Njombe imeshika nafasi ya pili kimkoa
ikiongozwa na Halmashauri ya Mji wa Makambako hatua ambayo imewafanya madiwani
hao kuona ulazima wa kupambana ili kufuta zero na daraja la nne katika shule
zote.
MWISHO
Comments
Post a Comment