Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
MPANGO wa Kuinua Elimu Nchini (EQUIP-T) unaotekelezwa katika
shule za msingi umetajwa kusaidia kuongeza ufaulu kwa asilimia 91 katika
mtihani wa darasa la nne katika mikoa tisa iliyotekeleza mradi huo kutokana na
kuimarisha stadi tatu za kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu, Ofisi ya Rais, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Gerald Mweli ameeleza mafanikio hayo
katika kikao cha wadau na wafadhili wa mradi huo walipokuwa wakifanya tathmini
ya mpango huo uliotekelezwa kwa miaka sita.
Amesema katika mpango huo
walimu wamefundishwa kutengeneza zana za kufundishia zinazopatikana kwenye
maeneo yao na kuwataka walimu kuondokana na dhana kwamba zana za kufundishia ni
lazima zinunuliwe.
Kwa upande wake Mratibu
Msaidizi wa mradi huo Mwalimu Joseph Katabalo amesema program hiyo ilianzishwa
katika mikoa ambayo ufaulu wake ulikuwa chini kwa miaka mitatatu mfululizo
kabla ya kuanza kwa program hiyo huku Ofisa Elimu Mkoa wa Tabora, Suzana Mwalubamba
akieleza mafanikio yaliyopatikana ambapo kuanzia mwaka 2014 kulikuwa na shule
700 na hadi sasa kuna shule 805 za msingi.
Mpango huo umetekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la
Uingereza (DFID) kwenye mikoa ya Kigoma,
Tabora, Shinyanga, Simiyu, Dodoma, Singida, Katavi, Mara na Lindi na Halmashauri 63.
MWISHO
Comments
Post a Comment