Wataalam wajengewa uwezo kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa utumbo ukiwa nje



Na. Lightness Mndeme, DAR ES SALAAM

Wataalam wa Afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila leo wamejengewa uwezo ili kuwasaidia kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa utumbo ukiwa nje.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto nchini Uingereza, Dkt. Naomi Wright 
akielekeza namna ya kumhudumia mtoto aliyezaliwa utumbo ukiwa nje

Ambapo takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili zinaonesha kuwa asilimia 100 ya watoto wanaozaliwa utumbo ukiwa nje hupoteza maisha kutokana na ukosefu wa elimu kwa watoa huduma za afya ya namna wanavyoweza kutoa huduma ya kwanza kabla ya kumfikisha mtoto katika hospitali zenye wataalam bobezi.

Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Zaituni Bokhari wakati wakutoa mafunzo hayo kwa njia ya vitendo yanayolenga kuwafikia watoa huduma za afya katika hospitali mbalimbali za rufaa ndani na nje ya Dar es Salaam.

“Tunatumaini kuwa mafunzo haya yatasaidia kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa utumbo ukiwa nje ambapo hadi sasa tayari madaktari na wauguzi wa MNH-Upanga na Mloganzila wamekwisha kupatiwa mafunzo na kuanzia kesho tutaanza kuzifikia hospitali mbalimbali za rufaa ndani na nje ya Dar es Salaam ili kuwapatia mafunzo haya,” amesema Dkt. Bokhari.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto nchini Uingereza, Dkt. Naomi Wright ametaja nchi nne ambazo zimechaguliwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto hao kuwa ni Tanzania, Ghana, Zambia na Malawi.

“Sababu hasa ya Tanzania kupatiwa mafunzo haya ni kutokana na ongezeko la vifo vya watoto wanaozaliwa matumbo yakiwa nje ambapo kwa nchi zilizoko kusini wa jangwa la Sahara ni zaidi ya asilimia 98%,” amesema Dkt. Wright.
Baadhi ya mafunzo yaliyotolewa ni pamoja na jinsi ya kumhudumia mtoto aliyezaliwa utumbo ukiwa nje, njia sahihi za kutoa huduma kwa mtoto huyo kwa kutumia mifuko safi ya plastiki na hatua za kufuata wakati wa kujiandaa kumtoa mtoto katika hospitali aliyopokelewa hadi kumfikisha katika hospitali yenye wataalam bobezi.

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.