Na. Jackline Kuwanda,
DODOMA
Afisa Masoko wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, James Yuna amesema kuwa kila mtu anapotaka kuomba eneo la kufanyia
biashara katika maeneo ya masoko kuna utaratibu unaotumika kwa lengo la kwenda
sambamba na matarajio ya Halmashauri na wao kuheshimu shughuli za biashara
zao ili ziweze kuwaletea tija.
Yuna aliyasema hayo jijini Dodoma wakati
akizungumza na Mtandao wa Dodoma News ofisini kwake leo kuhusu taratibu za
kupata eneo la kufanyia shughuli katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Afisa Masoko huyo amesema kuwa ipo
mikataba mbalimbali ambayo mfanyabishara hulazimika kuingia na Halmashauri
pindi anapohitaji kupata chumba kwa ajili ya kufanyia biashara kilichojengwa na
Halmashauri.
“Tutampa chumba cha biashara, lakini
tutampa mkataba wa upangaji ili aishi kwa uelewa wa mkataba huo na sisi tuwe
tunafahamu anaishi mle kwa maelekezo gani ili kuepuka mambo ambayo hayatarajiwi
kwenye maridhiano’’ alisema Yuna. Katika uwepo wa masoko katika Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, yapo makubaliano ambayo wamekuwa wakiyafanya na wafanyabiashara
wakati wanahitaji nafasi ya kufanyia biashara katika maeneo ya Masoko,
aliongeza.
“Kila mtu anapoomba eneo la biashara
katika Halmashauri ya Jiji, tunautaratibu ambao huwa tunaoutumia. Tunamueleza
kwanza atuandikie barua ili kuonesha nia yake kama anahitaji kupata eneo la
biashara katika maeneo ya masoko ambapo anaiandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Jiji la dodoma ili kuomba nafasi, na sisi tunakuja kuangalia nafasi zilizopo
na kuhakikisha tunampatia na kumtaka afanye biashara kwa mujibu wa mkataba’’ alisema
Yuna.
Katika hatua nyingine amesema kuwa uwepo
wa mkataba ni maridhiano ya pande zote mbili, huku akisema kuwa mikataba ina
umuhimu mkubwa kwa sababu inafafanua haki ya kila mtu kutoka pande zote mbili.
“Mikataba inafafanua haki za kila mtu
katika pande mbili kwa mfano mimi naweza nikawa nimekupangisha leo ukakuta
nimemuweka mtu mwingine ana haki ya kwenda kushitaki na kudai haki yake’’
alisema Afisa huyo.
Mbali na hilo amesema kuwa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma halina masharti magumu wanachokifanya ni kuwaelekeza
wafanyabishara licha ya kuwa na uwepo wa mikataba lakini kuna mambo mengi
ambayo wamekusudia kuwanufaisha ikiwemo kuboresha masoko ambayo wafanyabiashara
wataridhika nayo.
Hata hivyo, Yuna amesema ukishaingia
kwenye mkataba wanatakiwa kufahamu kuwa wako salama katika biashara zao
na hakuna mtu yeyeto atakaye wasumbua wala yeyote kuingilia biashara zao.
=30=
Comments
Post a Comment