Tanzania Yapokea Msaada wa Shilingi Bilioni 4.2 kutoka Japan


Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam

Tanzania imepokea msaada wa Yen za Japan milioni 200 sawa na Shilingi Bilioni 4.2 kutoka Serikali ya Japan kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James (kulia), na Naibu na Kaimu Balozi wa Japan nchini Tanzania, Katsutoshi Takeda, wakisaini mkataba wa Msaada wa Sh. 4.2 kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam


Mkataba wa msaada huo umesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Naibu na Kaimu Balozi wa Japan, Katsutoshi Takeda, kwa niaba ya Serikali ya Japan.
Katibu Mkuu, Doto James, alisema kuwa msaada huo utatumika kununua Meli ya Uvuvi yenye vifaa vya kisasa, mashine ya kutengeneza barafu, ghala la baridi la kuhifadhia samaki, Vifaa mbalimbali vya kuvulia samaki na vya karakana, gari lenye mitambo maalum ya barafu na Gari kwa ajili ya kusambazia samaki.
Alisema kuwa utekelezaji wa Mradi huu utachangia kwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano Awamu ya Pili (FYDP II), ambayo pamoja na mengine unalenga kuboresha Sekta ya Uvuvi na hatimaye kuvutia Watanzania zaidi kujihusisha katika Sekta ya Uvuvi kama shughuli kuu ya kujipatia kipato.
“Mradi huu utaongeza uuzaji wa samaki nje ya nchi, kuongeza uhakika wa chakula nchini, na pia utaboresha usindikaji wa samaki, kuongeza thamani na masoko na kupunguza upotevu wa mazao ya samaki baada ya kuvua”, alieleza James.
Alisema kuwa Kiwango cha ukuaji kwa shughuli ndogo za kiuchumi za uvuvi kilifikia asilimia 9.2 mwaka 2018 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 8.4 mwaka 2017 ambapo kiwango kikubwa cha ukuaji kilitokana na utunzaji mzuri wa mazalia ya samaki yakiwemo mabwawa ya watu binafsi sambamba na kuongezeka kwa mahitaji katika soko la ndani na nje.
James alisema kuwa, shughuli za uvuvi zilichangia asilimia 1.7 katika Pato la Taifa mwaka 2018, ambayo inadhihirisha umuhimu wa uvuvi katika uchumi, hivyo msaada uliotolewa utachangia jitihada za Serikali katika kufikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, Malengo Endelevu ya mwaka 2030 na Agenda ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063.
Alisema kuwa Serikali ya Japan imekuwa ikiisaidia Tanzania kupitia misaada na mikopo nafuu katika Sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Miundombinu ya barabara, Maji, Nishati Utawala Bora na Uwajibikaji ambapo mpaka sasa Jumla ya Sh. Trilioni 1. 3 zimetolewa na Serikali hiyo tangu mwaka 2012.
=30=

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.