Na.
Jackline Kuwanda, DODOMA
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto ametolea ufafanuzi juu ya kifo
cha Ustadhi Rashid Ally Mussa (62) ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya ‘The
Dalai Islamic Center’ na mmiliki wa shule ya ZAMZAM, mkazi wa Chang’ombe Extension
kuwa alifariki kutokana na tatizo la moyo kufeli na kushindwa kufanya kazi.
Akizungumza
na waandishi wa habari mkoani hapa, Kamanda Muroto amesema kabla ya kifo chake tarehe
21 Disemba, 2019 alihudhuria mkutano wa mahusiano ya dini mbalimbali huko jijini
Dar es Salam na kurejea Dodoma tarehe 22 Disemba, 2019 kwa kutumia usafiri wa
basi la kampuni ya Kimbinyiko na Baada ya kufika Dodoma alifika ofisini kwake
Mtaa wa Barabara ya Nyerere,kata ya madukani, akiwa ofisini kwake alipatwa na
tatizo la moyo kufeli hivyo alifariki kutokana na kukosa msaada wa haraka.
Wakati
huohuo Kamanda Muroto amesema kutokana na safari yake hiyo alikosa mawasiliano
na ndugu zake baada ya simu yake kuzima na kwa kuwa ndugu zake walifahamu
amesafiri waliendelea kumtafuta kwa njia ya simu bila mawasiliano.
“Pia
waliwasiliana na watu wengine aliokuwa nao katika safari hiyo hawakufanikiwa
kumpata hadi ilipofika tarehe 25 Disemba, 2019 majira ya saa 11.00 jioni, mtoto
wake alikwenda ofisini kwake na kukuta amefariki dunia na mwili wake ukiwa
umevimba, unatoa harufu na umeharibika kutokana na kukaa takribani siku nne’’ alisema
Muroto.
Amesema
Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na wataalamu wa uchunguzi wa matuko
kuchunguza tukio hilo ambapo eneo la tukio lilifanyiwa uchunguzi na upekuzi
katika ofisi yake na kugundua kuwa hakukuwa na uharifu wowote, hakuna wizi
kwani upekuzi ulifanyika na kukutwa begi dogo lenye nguo chache za safari, simu
yake ikiwa imezima, tiketi ya safari, pesa katika wallet shilingi laki mbili na
sitini (260,000) na vitambulisho vyake.
Katika
hatua nyingine amesema mwili wa marehemu ulipelekwa Hospitali ya Rufaa ya
Dodoma na kufanyiwa uchunguzi na Daktari na kuthibitisha kuwa sababu ya kifo
chake ni moyo kufeli na kushindwa kufanya kazi (Cardial arrest).
“Jeshi
la Polisi Mkoa wa Dodoma bado linaendelea kufanya uchunguzi kupitia simu zake
kubaini kama kuna taarifa za ziada’’ alisema Muroto.
Hata hivyo,
ametoa wito kuwa watu wasitumie taarifa za kifo hicho kupotosha umma au kuunda
taarifa zenye upotoshaji kama ambazo zinaenezwa mitandaoni.

Comments
Post a Comment