Na. Mwandishi Wetu, CHATO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Magufuli ameongeza siku 20 kwa watanzania kukamilisha zoezi
la usajili wa laini zao za simu kabla ya muda uliopangwa awali na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) kukamilika.
![]() |
| Rais Dkt Magufuli akibonyeza kitufe wkati akisajili laini yake ya simu kwa alama ya kidole |
Ongezeko hilo la muda alilitoa baada
ya kufanya usajili wa laini yake ya simu kwa alama za vidole jana wilayani
Chato, mkoani Geita.
Rais Dkt. Magufuli aliongeza siku
20 kuanzia tarehe Mosi Januari, 2020 hadi tarehe 20 Januari, 2020.
Aidha, aliwataka watanzania wote kusajili laini zao za
simu kwa alamu za vidole kama ilivyoelekezwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA).
Vilevile, alisisitiza kuwa muda huo ulioongezwa utakapokamilika
hakuna sababu nyingine itakayokubalika kwa mtu yeyote kutosajili laini yake.
Aliiagiza TCRA kuzima laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa baada ya 20
Januari, 2020.
![]() |
| Rais Dkt Magufuli katika kituo cha kusajili laini za simu |
Akiongelea
umuhimu wa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole, alisema kuwa ni muhimu
kwa usalama wa nchi. Usajili huo unaepusha vitendo vya utapeli na ujambazi
vinavyofanywa na wahalifu, ambao licha ya wengi wao kukamatwa na vyombo vya
dola wameendelea kusababisha usumbufu na upotevu mali za wananchi hususani
fedha.
=30=


Comments
Post a Comment