Na. Editha Edward -TABORA
Mtumishi mmoja katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora kitengo
cha ugawaji dawa anayejulikana kwa jina la Francis Mlesa (33) anashikiliwa na
Jeshi la Polisi Wilayani humo kwa tuhuma ya wizi wa a dawa zikiwemo za
ARVs.
Akizungumza na Blog hii Ofisini kwake, Ofisa Tarafa ya Igunga
mjini, Shadrack Kalekayo amesema tukio hilo lilitokea tarehe 24 Disemba, mwaka
huu ambapo mtumishi huyo alishitukiwa na mlinzi aliyekuwa zamu majira ya
saa Moja na nusu usiku baada ya kumuona amefunga maboksi mawili kwenye
baiskeli.
Kalekayo amesema baada ya kukagua maboksi hayo ilibainika kuwa
zilikuwemo dawa aina ya ARVs ila mtumishi huyo alifanikiwa kutoroka nazo baada
ya mlinzi kuzidiwa na watu wanaopita getini hapo.
Mlinzi aliyekuwa zamu siku hiyo Rushina Paulo alithibitisha
kumkamata mtumishi huyo na dawa hizo akidai kuwa zimeisha muda wake na akidai
kuwa alikuwa anaenda kuziteketeza ila mlinzi huyo alipoziangalia aliona kuwa
zilikuwa hazijaisha muda wake.
Amesema kuwa alitoa taarifa kwa uongozi wa Hospitali hiyo tarehe
26 Disemba, 2019 na alifikishwa mbele ya uongozi ambapo alikiri kuiba dawa hizo
huku akisema alizichukuwa kwa ajili ya kuziteketeza moto.
Kwa upande wa watumishi wa Idara ya Afya hospitalini hapo ambao
hawajataka majina yao yajulikane wamesema mtumishi huyo amekuwa akiwauzia
Wafanyabiashara wa Ng'ombe kwa ajili ya kunenepesha mifugo yao.
Kwa upande wake kamanda wa TAKUKURU Wilayani hapo Fransis Zuakuu
amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo huku akisema alipigiwa simu na raia wema
wakimjulisha kuwa kuna mtumishi ameiba dawa hospitalini na kutoroka nazo ambapo
baada ya kumtafuta na kumkosa alimwagiza Mganga mkuu wa Wilaya hiyo Deus Ruha
kumsaka ambapo Disemba 26 walimpata na tayari yupo mahabusu katika kituo cha Polisi
wilayani hapo.
Aidha, Nzuakuu ametoa wito kwa watumishi wa idara zote kufanya
kazi kwa uadilifu na kujiepusha na vitendo kama hivyo kwani Serikali
haitafumbia macho mtumishi Yeyote atakayebainika na vitendo kama hivyo vya wizi
wa dawa za Serikali.
Hata hivyo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Tabora ACP Barnabas
Mwakalukwa alipoulizwa juu ya tukio hilo amethibitisha kushikiliwa kwa Francis
Malesa huku akisema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala lolote kwani bado
wanaendelea kumhoji ili kubaini thamani ya dawa zilizoibwa.
=30=
Comments
Post a Comment