Na. Said Nguya, KAGERA
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally
ametoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na wilaya kuhakikisha wale waliofanya
kazi za ufundi, vibarua, wahudumu na kazi zingine katika miradi
mbalimbali ya serikali wanalipwa kwa wakati hasa kwa miradi ambayo serikali
tayari ilishatoa fedha hizo.
Dkt Bashiru amesema, kwa wale wasimamizi wa miradi hiyo ambao
wamekula fedha na kushindwa kuwalipa wafanya kazi kwa wakati, wakuu wa mikoa na
wilaya wasisite kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na warudishe fedha hizo
ili jasho la wananchi wanyonge lisipotee.
Bashiru ametoa maagizo hayo Desemba 27, 2019 alipotembelea na
kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Bukoba vijijini,
ambapo licha ya kuridhishwa na ujenzi huo lakini amekuwa akipokea malalamiko
mbalimbali ya wafanayakazi kutokulipwa kwa wakati licha ya fedha zote shilingi
bilioni 1.5 kufikishwa hospitalini hapo.
’’Natoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa nchi nzima,
kuhakikisha wanalinda miradi hii dhidi ya wadokozi na wezi wa rasilimali hizi
za wananchi, na wale wote waliotoa jasho lao kujenga miradi hii, yaani mafundi,
vibarua, wahudumu na wafanyakazi wengine, walipwe kwa wakati na jasho la
mwananchi lisipotee, kama kuna waliohusika katika kuchelewesha malipo yao,
wachuliwe hatua kali za kinidhanu kwa mujibu wa sheria za nchi.” Katibu Mkuu
amesisitiza.
Aidha, Dkt. Bashiru ametoa wito kwa wenyeviti wote wa vijiji na
mitaa nchi nzima kutoa ardhi kwa shughuli za jamii ikiwemo ujenzi wa Hospitali,
Shule, Ofisi za umma, n.k kama ambavyo imefanyika katika kijiji cha Kanazi kwa
wananchi kujitolea eneo ambalo ujenzi wa hospitali hiyo ya Halmashuri
unaendele, ambapo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za ujenzi wa
mradi huo.
Wakati huohuo, Dkt. Bashiru ametumia fursa hiyo kuwataka wanachi
kuendelea kuiamini CCM na serikali yake chini ya Mhe. Dkt John Pombe Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, ambapo ameweza
kudhibiti nidhamu katika serikali na Chama, na mafanikio yanayopatikana sasa ya
ujenzi wa hospitali nchi nzima, vituo vya afya, zahanati, barabara, madaraja,
umeme, miradi ya maji n.k ni matokeo ya jitihada hizo.
Ziara hiyo imejumuisha viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali
wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya Ndg. Evarist Babyegaya na Mkuu wa
wilaya Ndg. Deodatus Kinawiro
Katibu Mkuu yupo nyumbani kwake, Kagera wilayani Bukoba kwa
mapumziko ya siku kumi, ambapo anatarajiwa kumaliza mapumziko hayo mwanzoni mwa
mwezi Januari, 2020.


Comments
Post a Comment