CHANGAMOTO YA MIMBA KWA WATOTO KUKWAMISHA MIPANGO YAO


Na. Jackline Kuwanda, DODOMA
“Nilipata mimba nikiwa na umri wa miaka 15, na hiyo ilitokana na mimi kuwa naenda stendi kwa ajili ya kuokota mahindi ambayo tulikuwa tunaenda kuyasaga kwa ajili ya chakula ndipo kaka mmoja alianza kunipa hela na nikawa naenda kununua mahindi tunayasaga tunakula mwisho wa siku alinipa ujauzito  na aliukataa ujazito. Mama yangu baada ya kuona hayo alinifukuza nyumbani’’ alisema Julieth.

Julieth Bernad (sio jina lake halisi) ni mzaliwa wa Wilaya ya Chamwino katika Kata ya Manchali, mkoani Dodoma, anasema aliacha shule akiwa darasa la kwanza na hiyo ni kutokana na mazingira ya nyumbani kuwa magumu sana, baba yake na mama yake walitengana pindi yeye hajazaliwa.

Anasema baada ya mama yake kujifungua hali ya maisha kwao ilikuwa ni ngumu sana na ili wale chakula ilikuwa ni mpaka waendee kwenye michongoma na kutungua matunda yake ndipo wapate chakula na wakati mwingine ilikuwa wanaokota mahindi ndipo wale chakula.

“Tukawa tunamaisha mabaya sana, tuliendelea kuishi na mama yangu hivyo hivyo lakini mwisho wa siku nilipata ujauzito nikiwa na umri wa miaka 15 na nikazaa mtoto wa kiume” alisema Julieth.

Julieth anaendelea kusema kuwa hali iliyosababisha yeye kupata ujauzito na kujifungua mtoto wake wa kiume ni kutokana na hali ngumu ambayo ilikuwa nyumbani kwani hakukuwa na msaada wowote ule hivyo ili maisha yao yaendelee na wale alikuwa akienda stendi kwaajili ya kuokota mahindi ambayo walikuwa wakiyasaga kwaajili ya chakula ndipo kaka mmoja alianza kumpa hela kwaajili ya kununua mahindi, hapo ndipo mahusiano yalipoanzia na huyo ndiye alikuwa kama msaada kwake mwisho wa siku alijikuta ameshika ujauzito akiwa na umri mdogo.

Anasema baada ya yule kaka kumpa ujazito aliamuacha na hakujua ni kwaajili gani yule kaka amemuacha. “Aliniacha tu sijui aliona kwamba akinitunza atafanyaje kwa hiyo mimi sikuelewa inakuwaje baada ya yeye kuniacha na kwa sasa yuko mjini’’ alisema Julieth.  

Anasema wazazi wa mwanaume walikuwa wakitambua kuwa kijana wao amenipa ujauzito na walikuwa wakinisaidia pale ninapokuwa na shida licha ya kuwa kijana wao aliukataa ujauzito.

“Anaitwa Yohana Yusuph ni mkazi wa hapa Chalinze lakini kwa sasa yuko mjini  yeye alikuwa hafanyi kazi yeyote ile na hakuwahi kuniahidi kunioa’’ aliongeza Julieth.

Julieth anaeleza kwamba baada ya kijana huyo kukataa ujauzito alindelea na maisha yake wakati mwingine alikuwa akiuza maandazi lakini mama yake mzazi hakufurahishwa na hali ile ya yeye kushika ujazito aliamua kumfukuza nyumbani na aliendelea na biashara zake za kuuza maandazi, sambusa walau kidogo akawa anapata chakula.

“Wakati mama ananifukuza nilikuwa naujauzito nilikuwa bado sijajifungua na baadaye watu walimshauri nikarudi tena nyumbani hatimaye nikajifungua mtoto wangu lakini ilikuwa nikwa upasuaji kwa sababu umri wangu ulikuwa bado ni mdogo’’ alisema Julieth.

Anasema alipojifungua ndipo maisha yakawa magumu zaidi, mama yake alinifukuza tena na mtoto wake. Dada yake alimpatia nyumba akawa anaisha yeye pamoja na mtoto wake.

Julieth ni miongoni mwa watoto ambao wako katika mradi wa SAUTI yangu unaotekelezwa na shirika la utetezi wa wanawake na watoto la Women wake up (WOWAP) ambalo limedhamiria kuondosha vitendo vya ukatili kwa watoto. Anasema shirika  hilo limewasaidia kwa kiasi kikubwa, ameweza kujifunza kushona cherehani na anaendelea vizuri huku akielezea sababu inayopelea watoto wa kike ambao wako katika umri mdogo kuzaa mapema.

Nasra Suleiman ni Mratibu mradi wa SAUTI yangu unaotekelezwa na shirika la WOWAP, yeye anasema sababu inayopelekea watoto kupata mimba katika umri mdogo ni kutokana na hali duni za maisha ambazo watoto wamekuwa wakikutana nazo hivyo, hali hizo hupelekea watoto kutafuta namna ya kuweza kujikimu matokeo yake wanajikuta wanajiingiza katika vitendo ambavyo vinawasababishia madhara ikiwemo kushika ujauzito.

Lakini pia Nasra anasema uelewa mdogo wa hizo familia nao pia unasababisha kwa sababu wamekuwa na mtazamo kwamba mtoto wa kike bado anatakiwa kukaa nyumbani na kushindwa kumpa kipaumbe.

Ladislaus Loboto ni  Mtendaji wa Kijiji Mnchali B wilayani Chamwino anasema katika upatikanaji wa mimba na ndoa za utotoni  hali hiyo imejitokeza sana katika eneo lao na sababu kubwa ni kuwa na kipato duni.

“Hicho ndicho kinachosababisha watoto wanajiingiza katika vitendo ambavyo si vizuri, anaweza kupata shida yeyote ya chakula au hata mahitaji mengine muhimu hivyo anaweza kukubali kufanya ngono hata kwa shilingi mia tano” alisema Loboto.

Mradi wa SAUTI yangu ulianzishwa kutokana na maamuzi ya umoja wa mataifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya watoto kama ilivyoelekezwa katika malengo ya maendeleo endelevu na kutoka katika wito wa uwajibikaji kwenye muktadha wa ajenda ya maendeleo endelevu kufikia mwaka 2030.
=30=

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.