Na. Mwandishi Wetu, SUMBAWANGA
Viongozi wapya 2,766 wa vijiji na vitongoji walioshinda katika
uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika tarehe 24.11.2019 katika
wilaya ya Kalambo wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanatatua kero na
malalamiko ya wananchi wanaowahudumia katika vijiji na vitongoji ili kupunguza
msongamano wa wananchi wanaohitaji kutatuliwa kero zao katika ngazi ya wilaya
na mkoa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo muda
mfupi baada ya viongozi hao kula kiapo mbele yake na mbele hakimu wa mahakama
ya Wilaya ya Kalambo ambapo wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutoka katika kata
10 za tarafa ya Matai wilayani humo walishiriki katika kiapo hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongea na viongozi wapya wa vijiji na vitongoji muda mfupi baada ya viongozi hao kula kiapo. |
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongea na viongozi wapya wa vijiji na vitongoji muda mfupi baada ya viongozi hao kula kiapo |
“Katika ngazi hiyo ya vijiji, vitongoji na mitaa, wenyeviti wa
maeneo hayo mimi nikipata mtu anatoka kwenye vijiji vyenu analalamika kwa jambo
ambalo ni dogo sana, nitakuita. Utapata usumbufu wa kuja Sumbawanga, uhisabu
kuwa utatumia gharama zako kuja na kurudi kutoka kule kweny kijiji chako.
Nitakusumbua kwasababu wewe hutaki kusumbuka nikilipata tu nitakusumbua,
kwahiyo nendeni mkatatue kero za wananchi katika ngazi zenu, yako mambo mengi
mtusaidie sio kila kitu mkuu wa mkoa, kila kitu mkuu wa Wilaya na wengine
wanakwenda wanaandika mpaka kwa Rais,”Alisisitiza.
Aidha amewataka viongozi hao kuwaumikia wananchi wote bila ya
kujali vyama vyao vya kisiasa, dini wala kabila na kuwataka katika utekelezaji
huo kuwa shirikishi kwani wasipofanya hivyo wananchi watashindwa kushiriki
katika shughuli za kimaendeleo jambo litakalorudisha nyuma juhudi za mkoa
kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma stahiki na kwa wakati.
“Mambo ambayo mnapaswa kwenda kuyasimamia katika maeneo yenu kuwashirikisha
wananchi katika kupanga maendeleo, sio unakurupuka tu unasema mimi nataka hiki
kifanyike bila ya kuwashirikisha wananchi , lazima wapange waamue wao wenyewe
na wakishaamua wao wenyewe watashiriki katika kutekeleza lakini pia watasimamia
kulinda yale maamuzi yao na hiyo ndio demokrasia na hili ndilo mkalifanye kule,
viongozi wengine wakishachaguliwa kama hivi wanakuwa miungu watu, hatupendi
kuona miungu watu kwenye vijiji vitongoji na mitaa,” Alisema.
Na katika kuhakikisha viongozi hao
wanatekeleza majukumu yao bila ya visingizio amewaagiza wakurugenzi wote wa
halmashauri nne za mkoa huo kuwapatia mafunzo viongozi hao wapya pamoja na wale
ambao ni muhula wao wa pili au zaidi jambao litakalotawasaidia kutekeleza
majukumu yao kwa Mujibu wa Sera za Kisekta, Mikakati ya Kisekta, Sheria,
Kanuni, Miongozo na Taratibu zinazosimamia Sekta husika.
Wakati akitoa muhtasari wa taarifa
ya uchaguzi wa serikali za mitaa mratibu wa uchaguzi mkoa Albinus Mgonya
alisema kuwa mitaa 165 iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga imechukuliwa na
Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo ni sawa na asilimia 100 wakati katika ngazi ya
vijiji CCM imechukua vijiji 336 huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kikichukua vijiji 2 kati ya vijiji 339 vya mkoa wa Rukwa.
“Vitongoji vilivyoshiriki katika uchaguzi ni 1,816 na kwa nafasi
ya vitongoji Chama cha Mapinduzi kimepata nafasi 1,807 sawa na asilimia 99.4
Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimepata nafasi za wenyeviti wa vitongoji 8
sawa na asilimia 0.6. kwa faida ya wadau waliopo hapa nafasi hizi 8 mgawanyo
wake ni kama ifuatavyo, Sumbawanga Manispaa nafasi 1, Halmashauri ya Wilaya ya
Sumbawanga nafasi 1 na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi nafasi 6,” Alimalizia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo
Mh. Daudi Sichone wakati akitoa neon la shukurani aliwataka viongozi hao wapya
kuhakikisha wanawapatia elimu ya kutosha wananchi wanaowaongoza juu ya kutatua
kero na malalamiko katika ngazi hizo zao na sio kumshawishi mwananchi afike
ngazi mkoa.
“Hawa viongozi wetu wanantumia mkoa na taifa, hebu ifike mahali
tutoe elimu kwa wananchi wetu, kabla hajafika huko angalau akifika kule
ionekane sisi sote tunasapoti kwamba kwa tatizo lako hili ni vyema ukafika kwa
mkuu wa mkoa lakini sio tu unaamka tu na masimu yako unamyuhangaisha mzee wa
watu anashindwa kufanya kazi za watu,”Alisema.
Maeneo yaliyofanya uchaguzi katika mkoa wa Rukwa ni vijiji 67,
vitongoji 348, mitaa 9 na wananchi walioshiriki kupiga kura ni 118,887 huku
zoezi hilo la uchaguzi likiwa limefanyika katika hali ya amani na utulivu.
Comments
Post a Comment