Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, RUKWA
Wakala wa Barabara za mijini na Vijijini (TARURA) wametakiwa
kuhakikisha Barabara zote za Vijijini zinapitika mwaka Mzima kwa kufanyiwa
matengenezo na endapo itashindikana basi ni muhimu kuyapa kipaumbelea maeneo
korofi, hasa katika kipindi hiki cha Mvua jambo ambalo litawasaidia wananchi
kuendelea na shughuli zao za Kiuchumi bila vikwazo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
katika kikao cha Bodi ya barabara baada ya wabunge wa mkoa huo pamoja na
wenyeviti wa halmashauri kuilalamikia TARURA juu ya utendaji wake wa kazi
pamoja na mipangilio yao ya bajeti katika kutekeleza majukumu yao.
“Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA) kuhakiki Barabara zote
za vijijini katika Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa ili kwanza wawe na orodha
kamili ya Barabara za Vijijini na zipo kwenye hali gani,Baada ya
kuhakiki wawe na orodha ya Barabara zilizoingizwa kwenye Mtandao
wa Barabara za TARURA na Barabara zipi hazipo kwenye mtandao wa
Barabara za TARURA na kwanini?,” Alihoji
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimkabidhi zawadi ya pesa mmoja wa mtoto wa wananchi aliokuwa akizungumza nao kupata maoni juu ya ujenzi wa daraja la mto Kanteza katika mji mdogo wa Laela |
Aidha alisema kuwa kwa kufanya hivyo itawasaidia TARURA kuwa na
picha ya Barabara zote za Mkoa wakati wa upangaji wa Bajeti ya mwaka 2020/2021
ili waweze kuziweka kwenye Bajeti Barabara ambazo zinahitaji
Matengenezo.
Wakati wakiwasilisha malalamiko hayo miongoni mwa wabunge hao
walisema kuwa hawaridhishwi na bajeti inayotengwa na TARURA na hata hiyo
inayotengwa haifikishwi kwa wakati hali ambayo inasababisha hata hicho kidogo
kilichotengwa kushindwa kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mh. Ali Kessy alisema, “Tumepanga
bajeti milioni 400 wazilete zote milioni 400, hauwezi kupanga bajeti milioni
400 unaleta milioni 20, nimemuuliza mratibu wa (TARURA) Mkoa, mmeleta shilingi
ngapi anasema tumeleta milioni 20 kwenye bajeti ya serikali ya milioni 400,
walitenga kabia daraja la Kavunje, wakadarasai wamekwama daraja haliendelei na
mvua ndio hiyo kama unavyoona.”
Naye Mbunge wa Nkasi Kusini Mh. Desderius Mipata alisema kuwa
wananchi wa kata ya Ninde watatengwa kutokana na TARURA kushindwa kutenga
bajeti kwaajili ya ukarabati wa barabara inayowaunganisha wananchi wa kata hiyo
na kata za jirani.
“Kwahiyo naomba mtafute njia yoyote ya dharura ya kuwezesha eneo
hilo lipitike hakuna namna nyingine ya kufanya, nikiwa bungeni daraja la kwenda
ninde lilikuwa limevunjika, nikapiga kelele bahati nzuri walikuja wakatengeneza
kwa pesa kidogo lakini barabara yake haipitiki,” Alimalizia.
Wakati akitoa malalamiko yake kwa niaba ya wakandarasi wenzie
Bwana Anyosisye Kiluswa amesema kuwa wakandarasi bado wanazidai halmashauri
fedha za matengenezo ya barabara kadhaa kabla ya barabara hizo hazijahamishiwa
kwa TARURA na kuongeza kuwa halmashauri hizo zilishapewa fedha na serikali
lakini matokeo yake wametumia kwa matumizi mengine.
“Sasa kwa sasa hivi wakandarasi tunashindwa kutekeleza wajibu wa
kufanya kazi kwasababu pesa zetu wenyewe ni za kuunga unga, ukifanya kazi
umelipwa halafu pesa hiyo hiyo unaichukua unakwenda kufanya kazi sehemu
nyingine, sasa unapokuwa unafanya kazi bila ya kulipwa na nyingine ambazo zipo
wanazitumia kwenye maeneo mengine matokeo yake wakandarasi wa mkoa wa Rukwa
tunaonekana hatufanyi kazi vizuri,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Kaimu mratibu wa TARURA Mkoa wa Rukwa alisema
kuwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya fedha shilingi bilioni 4.133
kwaajili ya matengenezo ya barabara km 346.63 na vivuko 48 huku kutoka mfuko wa
barabara zikitengwa shilingi bilioni 1.763 kwaajili ya miradi ya maendeleo
ambapo daraja la mto Kavunja likitengewa shilingi milioni 400 na daraja la mto
Kanteza lilopo Laela likitengewa shilingi milioni 163.2.
Comments
Post a Comment