Leo tarehe 27 Novemba,
2019 Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira imeanza maandalizi ya mwongozo
utakaotumika kwenye ukaguzi wa migodi nchini.
Akizungumza katika
kikao cha maandalizi cha siku nne kinachoendelea jijini Dodoma,
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Dkt. Abdulrahman Mwanga amesema
lengo la mwongozo huo ni pamoja na kuwa takwa la Sheria na kupata taarifa
sahihi za kaguzi mbalimbali kwenye migodi.
Akizungumzia
namna shughuli zinavyofanywa na Kurugenzi yake, Dkt. Mwanga ameeleza kuwa,
Idara imekuwa ikifanya kaguzi mbalimbali kwenye migodi mbalimbali nchini lengo
likiwa ni kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini zinaendeshwa kwa kufuata
Sheria za Madini na Mazingira pamoja na kanuni zake.
Ameongeza kuwa, kati
ya maeneo yanayokaguliwa kwenye migodi ni pamoja na karakana, sehemu za
kuchenjulia madini, mabwawa ya topesumu, vyanzo vya maji n.k. ili
kuhakikisha hayaleti madhara kwa wafanyakazi wa migodi pamoja na wananchi
wanaoishi jirani na migodi husika.
Ameongeza kuwa
mwongozo wa ukaguzi wa migodi utaboresha kwa kiasi kikubwa kwenye shughuli za
ukaguzi wa migodi nchini.
Wakati huohuo
akizungumza katika kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa Huduma za Tume, William
Mtinya ameipongeza Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kwa hatua kubwa
kwenye uandaaji wa mwongozo husika kama utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tume
ya Madini.
Ameitaka Kurugenzi
kushirikisha wadau wengine ikiwa ni pamoja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na
kuongeza kasi ya ukamilishwaji wake ili uanze kutumika mara moja.
Aidha, Mtinya ameitaka
Kurugenzi kuhakikisha mwongozo husika unajikita kwenye uwekaji wa
mazingira mazuri ya biashara hivyo kuboresha ukusanyaji wa maduhuli.
Naye Kaimu Katibu
Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba mbali na kupongeza Kurugenzi
ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kwa maandalizi ya mwongozo husika, ameitaka
kutilia mkazo kwenye eneo la afya kwenye migodi pamoja na uboreshaji wa
kanzidata (database).
Aidha, wafanyakazi wa
Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wakizungumza kwa nyakati tofauti
mbali na kuwapongeza Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya
Samamba na Mkurugenzi wa Huduma za Tume, William Mtinya kwa kuwatembelea
wamesema kuwa wanaamini mwongozo husika utawarahisishia zoezi la ukaguzi kwenye
migodi mbalimbali nchini na kutoa taarifa sahihi.
Comments
Post a Comment